HALMASHAURI ya Mji kibaha imeanza ujenzi wa stendi kubwa ya kisasa ya mabasi yaendayo mkoani,
 itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.4.

Ujenzi huo unafanyika kutokana na stendi ya awali kuwa katika eneo la hifadhi ya barabara Kuu ya 
Dar es Salaam-Morogoro.

Ujenzi huo uko katika hatua za awali na utakuwa wa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza 
inatarajiwa kukamilka mwishoni mwa mwezi Desemba ama mwanzoni mwa Januari 2018.

Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Innocent Byarugaba, alifafanua ujenzi wa stendi hiyo
 unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa uendelezaji majiji na kuwa mkandarasi ni 
Kampuni ya MS Group Six ya Dar es Salaam.

Alisema stend hiyo ya kisasa itakuwa na uwezo wa kuingiza mabasi makubwa ya mikoani 60,
 mabasi ya kati 48, teksi 20, bajaji 10 na magari binafsi kwa ajili ya wanaopokea na
 kusindikiza wasafiri.

“Tunatarajia pia stendi hii itakuwa na jengo la utawala, mgahawa, ofisi za kukatia tiketi,
 kituo cha mafuta na miundombinu kwa ajili ya wenzetu wenye mahitaji maalum, lakini 
pia gereji kwa ajili ya kutengeneza magari yatakayokuwa yanaharibika,” alisema Byarugaba.

Pia itakuwa na mashine za kutolea fedha ATM, mahali pa kupumzikia abiria na kwa  awamu ya
 kwanza itakuwa na miundombinu iliyojitosheleza kuanza kutumika kwa maana ya uzio, 
kituo cha polisi, kizimba cha taka na miundombinu ya kukusanya ushuru .