Maisha ya siku hizi ni mipango. Bila mipango mizuri maisha mazuri ni ndoto, na maisha mazuri huanzia kwenye familia au nyumbani kwako. Ni raha sana kuwa na watoto. Ila raha hiyo haikamiliki bila watoto hao kuwepo kwa mpangilio maalum. Ni kweli kila mtoto anakuja na riziki yake lakini mmhhh……
Kitaalam mwanamke anatakiwa kuanza kuzaa akiwa na miaka 18 na azae kwa kupishanisha angalau miaka 3 ili aweze kupumzisha mwili wake na kujijenga kiafya. Changamoto kubwa huja kwenye hii miaka mitatu hii na ndipo baadhi ya wanawake hushindwa kabisa na kujikuta wanabeba mimba nyingine kabla ya muda huo kuisha.
JINSI YA KUZUIA MIMBA
Kuna njia nyingi sana za kuzuia mimba. Baadhi kati ya hizo ni;
1. Njia ya asili (Kufuata kalenda au mzunguko wa hedhi)
2. Mwanaume kumwagia manii nje
3. Kutumia kinga (kondomu) kila mara mnapofanya mapenzi
4. Kutumia vipandikizi (Njia ya vijiti)
5. Kuchoma sindano ya dawa za kuzuia mimba
6. Kutumia vidonge vyenye dawa za kuzuia mimba
7. Kufunga kizazi
Leo tuzungumzie hizo njia namba 5 na 6.
Kuna dawa mbalimbali ambazo hufanya kazi ya kuzuia mimba isitungwe. Dawa hizo hufanya kazi kwa kuingilia ufanyaji kazi wa homoni za uzazi ambazo ni Oestrogen na Progesterone. Matokeo yake ni kwamba mayai hayawezi kupevushwa, mbegu za kike na za kiume haziungani na mimba haitungwi.
Kuna dawa zenye Oestrogen peke yake, zenye progesterone peke yake na zenye mchanganiko wa oestogen na progesterone.
Dawa hizo ni pamoja na Levonergestrel, Medroxyprogesterone, ethinylestradiol na norethisterone.
Dawa hizo ndizo tunazomeza kama vidonge kila siku au kuchomwa sindano za kupanga uzazi.
MAMBO YA KUZINGATIA
i. Usianze kutumia dawa hizi bila kupata ushauri wa daktari. Ni lazima kujadili mtindo wako wa maisha na hali yako ya kiafya kisha kujua dawa gani zitakuwa nzuri zaidi kwako na njia gani itakuwa nzuri zaidi kuzitumia. Tumia dawa zinazoendana na hali yako, mwili wako na mtindo wako wa maisha
ii. Ufanisi wa dawa za kuzuia mimba hutegemea sana jinsi zitakavyotumika. Kwa vidonge vya kawaida vya kumeza kila siku ni vyema mwanamke akameza kila siku wakati wa asubuhi tena saa ile ile. Dawa hizi zinaingiliana na dawa nyingine na ufanisi wake huweza kupungua, kwa hiyo kila mara unapokuwa unapewa dawa za magonjwa mengine hospitali toa taarifa kama unatumia dawa za uzazi wa mpango.
Tumia dawa hizi vizuri zaidi ili kuweza kupata matokeo mazuri. Vinginevyo unaweza kupata mimba hata kama utakuwa unazitumia.
iii. Kwa mama ambaye anaendelea kunyonyesha dawa nzuri zaidi kwake ni zile za progesterone kama vile Levonergestrel au norethisterone. Mama anayenyonyesha ni vyema apate ushauri wa daktari mara kwa mara
iv. Endapo utakuwa umefanya mapenzi siku ambayo haukuwa katika dawa hizi ni vyema kupata ushauri wa kitaalam haraka iwezekanavyo na kutumia dawa ya dharura ya kuzuia mimba utakayoshauriwa na daktari
Pata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa yoyote
0 Comments