Mshambuliaji wa zamani wa kalbu ya Simba Athumani Machupa ambaye amewahi hucheza soka la kulipwa nchini Sweden ameamua kurudi Tanzania na moja kwa moja atajiunga na klabu ya Friends Rangers inayocheza ligi daraja la kwanza Tanzania bara.
Inawezekana ikawa ni jambo la kushangaza kwa mchezaji ambaye ametoka Ulaya kwenda moja kwa moja ligi daraja la kwanza wakati angeweza kucheza ligi kuu Tanzania bara kwa misimu kadhaa kabla ya kushuka kwenda daraja la kwanza. Machupa ametoa sababu zake za msingi za kuamua kucheza Friends Rangers
“Nimeangalia kasi yangu na kasi ya ligi daraja la kwanza nadhani naweza kuendana nayo ndio maana nimeamua nicheze huko kuliko kukimbilia ligi kuu”-Machupa.
“Nataka kuisaidia Friends Rangers kwa sababu ndio klabu iliyonilea tangu nikiwa mdogo, nilianza kuonekana nikiwa pale kabla ya kujulikana sehemu yoyote. Kwa hiyo mimi kurudi Rangers ni sehemu ya kuisaidia klabu yangu kutokana na uzoefu nilionao wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha timu inafanya vizuri.”
“Nikiwa Rangers nataka kusaidia vijana  kutimiza malengo yao kwa kushirikiana na familia zao. Nitajihusisha sana na vijana wa umri kuanzia miaka 15, sio kwamba nitakuwa nawasidia kwa pesa bali nitakuwa nawapa miongozo, kwa sababu tayari nina uzoefu ninaweza kwenda sehemu ambayo mtu mwingine hawezi kwa ajili ya kufanikisha jambo fulani kifupi nitakuwa kama meneja.”
Fundi huyo wa kupasia kamba amesema hajafikiria kuingia kwenye ukocha kwa sababu tayari Friends Rangers wameimepanga kumsaidia mchezaji wao wa zamani Jabir Aziz kusomea ukocha ili badae aisadie timu.
“Kwa sasa tunamuandaa Jabir Aziz Stima kuwa kocha na tayari huwa anakaa na vijana na kuwaelekeza baadhi ya mambo, kwa kuwa bado anacheza ligi anakuwa na mambo mengi lakini atakapomaliza soka ataingia rasmi kwenye ukocha.”